Tuesday, September 11, 2012

SIMBA YATWAA NGAO YA HISANI,WASEMA WANAIHOFIA YANGA TUU!

 
Nyamlani akimpa mkono wa pongezi Akuffo. Anayemfuatia ni Waziri Mahanga, akiwasubiri Ngassa na Komabil Keita
Kushoto Kaseja, kulia Ngassa na Akuffo wakicheza kiduku   
Hatari kwa kwenye lango la Simba, Kaseja chini kule

SIMBA SC, inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetwaa Ngao ya Jamii, baada ya kuifunga Azam FC, mabao 3-2 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar e s Salaam.
Shujaa wa Simba leo hii alikuwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto aliyefunga bao la ushindi dakika ya 78 kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa wa Azam, Deo Munishi ‘Dida’ amekaaje.
Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na kipre Herman Tchetche, wakimtungua kipa namba moja Tanzania, Juma Kaseja.
Bocco alitangulia kufunga dakika ya tano ya mchezo huo, baada ya kupigiwa kona fupi na Abdi Kassim ‘Babbi’, akatoa pasi kwa Abdulhalim Humud ambaye alimrudishia mfungaji huyo akafumua shuti kali la chini likajaa nyavuni pembezoni mwa lango kulia.
Bocco ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba SC leo, alimtoka Amir Maftah upande wa kulia wa Uwanja na kuingia ndani kabla ya kutoa krosi fupi kwa Kipre aliyemtungua Kaseja na kuipatia Azam bao la pili dakika ya 35.
Simba ilipata bao lake la kwanza dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mfungaji Daniel Akuffo kwa penalti, baada ya Said Mourad kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha pili Simba walirudi na nguvu zaidi na kuamua kushambulia kwa mipira ya pembeni, ikiwatumia Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi ambao walikuwa wakibadilishana reli.  
Kwa staili hiyo, haikushangaza Simba ilipotumia dakika 45 za mwisho kwa kufunga mabao mawili yaliyowatoa nyuma kwa 2-1 na kuibuka kidedea kwa ushindi wa 3-2.
Emanuel Okwi alimchambua kama karanga Erasto Nyoni na kuingia ndani kabisa akiwatoka mabeki wengine wa Azam, kabla ya kuujaza mpira nyavuni kwa shuti kali na Kazimoto akamaliza kazi dakika ya 78.
Kwa ujumla katika mchezo huo, Azam ilitawala kipindi cha kwanza na ilikosa mabao mawili zaidi ya wazi kupitia kwa Himid Mao na Kipre, lakini kipindi cha pili Simba walitawala mchezo na kama wangekuwa makini, nao wangeweza kuvuna mabao zaidi.  
Naibu Waziri wa Kazi, Makongoro Mahanga alimkabidhi ngao Nahodha wa Simba, Juma Kaseja baada ya mechi hiyo, ambaye alikwenda kushangilia na wachezaji wenzake na mashabiki wa timu hiyo.   

No comments:

Post a Comment