Ngassa kushoto akizungumza na Mwenyekiti wa Yanga, Manji
Na
Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Mrisho Khalfan Ngassa
amepiga hodi Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kupinga kuuzwa
kwake katika klabu hiyo, akitokea Azam FC bila kuhusishwa.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Ngassa amesema
kwamba hajafanya mazungumzo na Simba SC wala Azam FC juu ya uhamisho. “Mimi
sijui chochote, na sikatai kuhamishwa, kwa sababu mimi soka ni kazi yangu na ninaweza
kucheza popote, ila taratibu zifuatwe tu,”alisema.
Ngassa amesema baada ya kuona mambo yanakwenda
kinyume cha utaratibu, ameamua kulifikisha suala lake Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji ili haki itendeke.
Mapema jana, Azam ilimuuza kwa Sh. Milioni 25 kwa
klabu ya Simba na sasa Mrisho anafuata nyayo za baba yake Khalfan Ngassa,
ambaye aliichezea Simba SC 1991/1992.
Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya
mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya
Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa
mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa
bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba
wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la
Sh. Milioni 55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na
kwa Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata akiwa
kwa Wekundu wa Msimbazi.
Mapema jana mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza
wa Azam FC jana alifukuzwa katika klabu
hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga
Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani
ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi
ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo
na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa
anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya
Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na
kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na
kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mbali na Ngassa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ naye
pia alikkuwa katika wakati mgumu na juzi inadaiwa alionekana akilia wakati
anazungumza na kiongozi mmoja wa Azam, akiuliza ni lipi kosa lake. Hata hivyo,
vyanzo vinasema Sure na Azam wamemalizana salama na wataendelea kuwa pamoja.
Sure Boy, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana
ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ juzi na jana hakufanya mazoezi, lakini leo ameanza.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne
kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin,
Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji
na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
No comments:
Post a Comment