Sure Boy arudi kazini
Na
Prince Akbar
SALUM Abubakar ‘Sure Boy’ amemalizana salama na
uongozi wa Azam FC, ambao umejiridhisha mchezaji huyo hakuhusika kwa namna
yoyote kuihujumu timu hiyo katika fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame, dhidi ya Yanga, Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Chanzo cha habari kutoka Azam kimesema kwamba, baada
ya mazungumzo marefu kati yake (Sure Boy) na wamiliki, imekubalika mtoto huyo
wa winga wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ alisukumiwa ‘Jumba bovu
tu’.
“Sure alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotoroka
kambini usiku wa siku ya kuamkia mechi na Yanga, lakini alikuwa hajui chochote.
Na hakuhusika, ila ameomba radhi na amesamehewa na hivi ninavyokuambia yupo
hapa mazoezini,”kilisema chanzo chetu leo.
Azam wanaendelea na mazoezi chini ya makocha wake wa
muda, Vivek Nagul kutoka India na Muingereza Kali Ongala, baada ya aliyekuwa
Kocha Mkuu, Stewart Hall kufukuzwa kazi juzi.
Stewart amefukuzwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya
Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho katika mechi ya fainali ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati
ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa
kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya
kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0
No comments:
Post a Comment