Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji
Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri
ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana leo (Januari 22
mwaka huu) kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya
kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali
maalumu kutoka FIFA.
Okwi
ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia
aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional
permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi
ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
Katika
FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi
ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel
imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du
Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola
za Marekani 300,000.
Hivyo,
TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza
Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika
shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.
No comments:
Post a Comment