KARIBU KATIKA BLOG HII YA KIJAMII



dstv

blog

Thursday, August 2, 2012

ASUBUHI YA VILIO CHAMAZI, HADI KOCHA MUHINDI AMWAGA MACHOZI WAKIMUAGA STEWART

 
Wachezaji wa Azam
Na Prince Akbar
WACHEZAJI wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo, pamoja na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, asubuhi ya leo wameangua kilio, tena kile cha kamasi wakati wakimuaga aliyekuwa Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Muingereza Stewart Hall ambaye alifukuzwa rasmi jana.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi asubuhi ya leo, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa, aliyeongoza ni Jemedari Said na makocha ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati anaagana na family yake, aliyoishi kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo na mafanikio.
Stewart alifukuzwa jana katika klabu hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha juzi cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa kwa ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana, akisaidiwa na Kali Ongala.
Imeelezwa baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.

No comments:

Post a Comment